islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


HAKI ZA MUISLAMU JUU YA MUISLAMU MWENZAKE KATIKA UISLAMU


14931
wasifu
Udugu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayoishusha kwa Waumini wa kikweli. Udugu ni kinywaji safi ambacho Mwenyezi Mungu Anawanyesha Waumini wasafiwa. Uislamu ulihimiza kuyatilia nguvu mafungamano ya Muislamu na nduduye Muislamu, Akayawekea hilo mambo yenye kutilia nguvu mafungamano hayo, kama vile kutoa salamu,kutazama mgonjwa na yasiyokuwa hayo miongoni mwa haki za Muislamu kwa nduguye Muislamu.
Khutba ya

Enyi Waislamu,Uislamu ni dini kubwa imeweka muongozo ambao kwamba inakusanya haki na uwajibikaji, miongoni mwa haki hizo ni haki ya Muislamu juu ya Muislamu mwenzake. Lengo kubwa ya haki hizi ni kuleta mapenzi na udugu wa kiislamu. Kila Muislamu akijua haki yake na ya mwenzake, basi itakuwa ni wepesi Waislamu kushikamana na kuwa kitu kimoja.

Uhakika wa udugu katika dini

Umma wa kiislamu leo umekuwa kama povu la bahari, umevunjika nguvu zake na kuwa wanyonge. Na ulimwengu hauna heshima isipokuwa watu wenye nguvu. Na sababu ya kudhoofika umma wa kiislamu ni kufarikiana kati yao. Na nguvu ni matunda ya umoja na mapenzi na haukudhoofika umma huu ila baada ya kukosa umoja nao ni udugu.

Uhakika wa udugu ni pale Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alipounganisha maswahaba walipokuwa Makkah pamoja na kuhitalifiana rangi zao na maumbile yao na ndimi zao na malengo yao ya maisha. Amemuunga Hamza ambaye ni mkureishi na Salman ambaye ni mfursi na Bilal ambaye ni mhabasha na Suheib ambaye ni mrumi na wote wakawa wanaimba qaswida hii: Uislamu ndio baba yangu Wakijifakhiri kwa kabila la Qais au Tamim. Na wote walikuwa karibu na Neno lake Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالى :(إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ)

[الحجرات: 10]

{{Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na Mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe}}. Hii ndio daraja ya kwanza katika udugu wa kiislamu, kisha Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akaunganisha watu wa Madina amabao ni kabila la Aus na Khazraj baada ya kupigana vita muda mrefu kati yao.

Kisha Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akaunganisha watu wa Makka (waliogura) na watu wa Madina. Kulipatikana tukio ambalo halina mfano kwa mwanadamu. Amepokea Anas hadithi akisema: [ Alikuja AbdurRahman bin ‘Auf kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akamuunga na Sa’ad bin Rabiya na alikuwa na mali nyingi, akasema Sa’ad: nitakugawiya nusu ya mali yangu na nitakupatia mmoja kati ya wake zangu. Tazama anayekupendeza zaidi nimuache. Akasema AbdurRahman Mwenyezi Mungu akubariki, (nionyeshe soko)]. Kwa sasa hatuwezi kupata mfano wa Sa’ad!?. Mmoja wa watu wema alisema: Wako wapi wanaotoa mali yao usiku na mchana, siri na dhahiri akajibiwa: Wameenda pamoja na wasioomba watu wakafanya ung’ang’anizi. Enyi Waislamu haki ya Muislamu kwa Muislamu mwenzake ni kumpenda kwa ajili ya Mungu. Amepokea Anas Bin malik akisema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mambo matatu mtu akiwa nayo anapata imani; moja wapo ni kumpenda mtu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu].

Miongoni mwa Haki ya Muislamu Juu ya Muislamu Mwenzake

Kupendana kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Taala). Amepokea Abu Huraira hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema watu saba watafunikwa na kivuli siku ya kiama ambapo itakuwa hamna kivuli; mmoja wao ni watu wawili wapendanao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wameshikana kwa ajili yake Mwenyezi Mungu na wakatengana kwa ajili yake Mwenyezi Mungu.

Kutembeleana kwa lengo ya kujuana hali. Amepokea Abu Huraira hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema [Mtu alimtembelea ndugu yake katika kijiji kingine Mwenyezi Mungu akamtuma Malaika kwa sura ya binadamu, akamuuliza waenda wapi? Akasema: naenda kumtembelea ndugu yangu. Akasema: Je ana neema unayotarajia (kutoka kwake)? Akasema: Hamna neema yoyote, isipokuwa nimempenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Akasema Malaika: Mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu nimetumwa kwako. Jua Mwenyezi Mungu anakupenda kama unavyompenda ndugu yako].

Kuitikia Salamu. Amepokea Abu Dawud akisema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) [Mguu hautoingia peponi mpaka muamini, na hamtomuamini mpaka mpendane. Je Nikujulisheni jambo mkilifanya mtapendana? Toleaneni salamu kati yenu].

Kufuata janeza na kwenda mazikoni. Amepokea Abu Huraira hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema: [Haki ya Muislamu juu ya Muislamu mwenzake ni sita kumsalimu pindi ukikutana nae, kuitikia wito anapo kuita, kuchukua nasaha yake anapo kunasihi, akichemua kumuambia Mwenyezi Mungu akurehemu, kumtembelea anapokuwa mgonjwa, kumzika anapokufa].

Kutokuwa na chuki. Anas amepokea hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Msichukiane, msifanyiene vitimbi, msishindane, kueni ndugu katika waja wa Mwenyezi Mungu]. Hasadi ni maradhi hatari jee huridhiki kwa aliyegawanya riziki ambaye ni Mwenyezi Mungu. Inapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu yeye ndiye mtoaji. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَالَّذِينَ جَاءُوا مِنْ بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَان) [الحشر: 10]

{Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu Tusamehe sisi na ndugu zetu waliotangulia katika Uisalmu}}.

Amepokea Anas akisema: Ilikuwa tumekaa pamoja na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akasema Mtume: [Atakuja mtu wa peponi, akatokea mtu wa Answaar ndevu zake zilikuwa safi, na ameshika vitu vyake kwa mkono wa kushoto. Na siku ya pili Mtume akasema hivyo hivyo, na akatokea mtu yule yule hata siku ya tatu. Abdullah bin Amru akamfuata nyumbani kwake na akawa naye muda wa siku tatu, wala hakumuona akisimama usiku isipokuwa akishtuka usiku humtaja Mwenyezi Mungu katika kitanda chake mpaka ikifika swala ya alfajiri. Na alikuwa hamsikii isipokuwa akizungumza maneno ya kheri. Akamsimulia ‘Abdallah Bin ‘Amru sababu ya kumfuata kwa kuwa wewe ni mmoja kati ya watu wa peponi. Akasema: sina chuki na Muislamu yoyote].

Kumsaida Muislamu mwenzake akiwa na shida. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mwenye kumsaidia Muislamu kwa kumuondoshea shida. Menyezi Mungu atamsaidia kumuondoshea shida ya siku kiyama. Na mwenye kumfanyia wepesi mtu mwenye uzito. Mwenyezi Mungu Atamfanyia upesi duniani na kesho akhera. Na mwenye kumsitiri ndugu yake Muislamu duniani na kesho akhera, Mwenyezi Mungu Atamsitiri dunuani na kesho akhera].

Kumnusuru Muislamu sawa akiwa amedhulumu au amedhulumiwa. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mnusuru ndugu yako anayedhulumu au anayedhulumiwa. Akasema mtu: tunamnusuru anayedhulumiwa, lakini vipi tunamnusuru anayedhulumu? Akasema Mtume: ni kumzuia anapodhulumu].

Kusitiri aibu ya Muislamu na kumuombea Mungu msamaha kwa kosa lake. Kweli ndugu yako si Malaika wala si nabii kwani yeye ni mwanadamu.

Wamesema wanavyuoni: Watu ni aina mbili:-

Watu wanaojulikana kwa wema na kuepukana na maasi, basi wakikukosea unapaswa kusitiri na kutofunua aibu yake.

Watu wanaofanya maasi kwa uwazi wala hawamuonei haya Mwenyezi Mungu, hao ni waovu.

Khutba ya pili

Ndugu zangu Waislamu mafungamano ya uhakika ni mafungamano ya dini ambayo kwamba unafunga jamii kuwa kama mwili mmoja na pia kama jengo moja. Ndugu zangu Waislamu inapaswa juu yetu kusaidiana na kuwa ndugu moja.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى :(وَأَطِيعُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ وَاصْبِرُوا إِنَّ اللَّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ) [الأنفال: 46]

{{Wala msizozane (msigombane), msije mkaharibikiwa na kupotea nguvu, na vumilieni. Bila shaka Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaovumilia}}. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

وقال تعالى) وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا) [آل عمران: 103] {{Na shikamaneni kwa kamba (dini) ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msiachane}}.

Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kuweni ndugu katika waja wa Mwenyezi Mungu, mcheni Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na watu waliokuwa pamoja. Na umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Dini ya Kiislamu imewakataza waumini kuzozana na kubishana baina yao, kufanya hivyo, ni sababu ya umma kukosa nguvu na kuwa dhaifu mbele ya maadui. Umoja wetu na kupendana kwetu ni kushikamana na Kitabu cha Allah na mafundisho ya Sunna ya Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Mwisho

Ndugu katika imani, Msingi mkubwa wa kushikamanisha Umma na kuwa kitu kimoja ni udugu wa Kiislamu. Bila ya udugu wa kiislamu hatuwezi tukakushikamana. Na udugu unaanza chini kuanzia familia ndogo kupendana kwa ajili ya Allah, isiwe ni kwa ajili ya nasaba, kisha mapenzi katika jamii na baadae umma wote. Ni wajibu juu yetu kufuata mfumo wa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika kuleta udugu wa kiislamu. Ni lazima tufundishe familia zetu na jamii ya kiislamu mapenzi na udugu kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Taala). Tukifanya hivyo, tutaweza kurejesha utukufu wa Dini ya kiislamu na kusimamisha serikali ya kiislamu.

Tumuombe Mwenyezi Mungu azidishe mapenzi baina yetu kwa ajili yake, na atuepushie na kila sababu ya kuchukiana na kutengana.





Vitambulisho: