islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


KUPEANA NASWAHA NA UAMINIFU KATIKA UISLAMU


6421
wasifu
Kutoa ushauri mzuri ni msingi wa Dini na shina lake. Kwani Dini ni ushauri mzuri. Na ushauri unakuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa Waislamu na wale wa kawaida. Mja anapotoa ushauri katika mambo haya huwa amejikamilishia dini yake. Na mwenye kuwa na kasoro katika kutoa ushauri katika jambo lolote miongoni mwa hayo, Dini yake huwa imepungua kwa kiasi cha kasoro aliyoifanya. Ni juu ya Muislamu atunze uaminifu katika kutoa ushauri wake na aseme haki bila mapendeleo kwa mtu yoyote, kwani yeye anaaminiwa mbele ya ya Mwenyezi Mungu
Khutba ya

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetuamrisha kukumbushana na kupeana nasaha katika mambo ya Dini yetu. Huku tukimtakia rehma na amani Mtume wetu Muhammad aliyekuwa mtoaji nasaha nambari moja vile vile mkweli mwaminifu.

Enyi Waislamu ! watukufu! Mazungumzo yetu ya leo ni kuhusu maudhui muhimu anayohitaji Muislamu katika maisha yake nayo ni nasaha, na nasaha ni kumtakia kheri apewaye nasaha. Tukijua ya kwamba nasaha ni msingi mkubwa wa dini, bali Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema kwenye hadithi yake: [Dini ni nasaha, Dini ni nasaha, Dini ni nasaha. wakamuuliza maswahaba: ‘Kwa nani ewe Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akasema : Kwa Mwenyezi Mungu na kitabu chake na Mtume wake na viongozi wa kiislamu na Waislamu kwa jumla].

Faida tunazozipata katika hadithi hii ni kule kuonesha ya kwamba nasaha ina daraja ya juu kabisa, na faida nyingine kutajwa sehemu ambazo nasaha hupatikana. Sehemu hizo ni nasaha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka nayo ni kufanya ibada kwa ajili Yake pekee na kutaka radhi Zake. Ama nasaha kwa kitabu chake ni kukisoma na kufuata maamrisho yaliyomo na kujiepusha na makatazo yaliyokatazwa ndani ya Kitabu hicho na kuziamini khabari zilizomo ndani yake. Ama nasaha kwa Mtume wake ni kumpenda na kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake na kuitetea heshima yake akiwa hai au akiwa amekufa. Ama nasaha kwa viongozi kuwaunga mkono kidhati kuwapa nasaha kwa maslahi ya umma katika ulimwengu wao na akhera yao. Pia kuwasikiliza na kuwatii katika mambo mema na kuitakidi kwamba ni lazima kufuata maamrisho yao ikiwa hawakuamrisha maasi. Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

فقال تعالى): يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنْكُمْ) [النساء: 59]

{{Enyi mlio amini mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na viongozi katika nyinyi}}. Ama nasaha kwa Waislamu wa kawaida ni kuwapendea kheri na kuwaepushia uovu vile vile kuyazungumza mazuri yao na kuyaficha maovu yao na kuishi nao kwa upendo na udugu. Pia kuwasaidia endapo wanadhulumiwa. La kusikitisha ni kwamba Waislamu wamepuuza suala zima la kupeana nasaha. Tukijua ya kwamba kulipuuza suala hili ni kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na hasara yake ni kubwa duniani na kesho akhera.

Sifa za Mtoaji Nasaha

Kuna mambo yatakiwa yazingaziwe na yafuatwe katika kadhia nzima ya nasaha Kati ya mambo hayo ni kama yafuatayo:

Ni lazima nasaha iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala), na isiwe kwa ajili ya kutaka sifa au kuonekana na watu. Mola (Subhaanahu wa Taala), Amesema:

قال تعالى) : وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ) [البينة: 5]

{{Na hawakuamrishwa isipokuwa wamuabudu Mwenyezi Mungu hali ya kumtakasia yeye ibada}}.

Ni lazima awe mtoaji nasaha ni mjuzi wa yale anayoyazungumza.

Ni lazima mtoaji nasaha awe mwaminifu. Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema akizungumza kuhusu Mtume Huud :

قال تعالى حكاية عن هود عليه السلام (أُبَلِّغُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَأَنَا لَكُمْ نَاصِحٌ أَمِينٌ )

[الأعراف: 68] {{Nafikisha ujumbe wa Mola wangu na mimi kwenu ni mtoaji nasaha mwaminifu}].

Nasaha iwe kwa njia ya siri kwa kiongozi na raia, lakini ikishindikana basi hakuna ubaya ikiwa wazi na khaswa ikiwa ni mambo yaliyo kinyume na sheria waliyo kubaliana wanachuoni wote kwamba ni haramu.

Haishurutishwi kwa mtoaji nasaha awe mwanachuoni mkubwa na wala si lazima awe mwadilifu zaidi kuliko anayepewa nasaha. Amesema Imam Ishaaq Ibn Ahmad katika Utangulizi wa nasaha kumwandikia Ibn Al-Jauzia Mwenyezi Mungu awarehemu: ‘Kama ingekuwa hakatazi ovu aliye na elimu chache kumkataza mwenye elimu nyingi ingekuwa watu hawakatazani maovu na tungekuwa kama Bani Israail pale Mwenyezi Mungu Aliposema: ”Walikuwa hawakatazani maovu waliyokuwa wakiyafanya’.

Enyi Waislamu ! Lau atafuatilia Muislamu hali za wema waliotangulia ataona vipi walipigiwa mfano katika kutoa nasaha na kuzikubali. Napenda nitaje mifano miwili nadhani itatosha:

Amesema Abubakar Swiddiq, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “ Hana kheri katika sisi asiyekubali nasaha na hana kheri katika nyinyi asiyeitoa nasaha”.

Amesema ‘Umar ibn Khattwab radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “ Mwenyezi Mungu amrehemu mtu aliyeniletea zawadi ya aibu zangu”.

Enyi waumini! Tujibidiisheni katika kutoa nasaha. Na tumtakasie Mwenyezi Mungu katika kadhia nzima ya kutoa nasaha.Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie miongoni mwa wanaosikiliza mema na wakawa ni wenye kuyafuata.

Khutba ya pili

Umuhimu wa Kutekeleza Amana.

Shukrani za dhati ni za Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala), na rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad. Enyi Waislamu! Mwanzo kabisa maana ya amana ni kulazimiana mwanadamu na haki ya Mwenyezi Mungu na ibada yake kama alivyoamrisha hali ya kumtakasia yeye ibada.

Ndugu katika imani! Ametuamrisha Mola kutekeleza amana na sehemu ambazo amana hupatikana. Miongoni mwa sehemu hizo ni kusimamisha Swala. Kwani Swala ni amana na atakayeipoteza Swala basi isiyokuwa swala ni wepesi zaidi kuipoteza. Zaka pia ni amana. Pale alipowapiga vita Abubakar Swiddiq radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, waliokataa kutoa zaka inaonesha kwamba yeye aliichukulia zaka kuwa ni jukumu muhimu la Dini, na kuwa wale waliokataa kutoa wameritadi. Saumu pia ni amana. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [ kiwa mmoja wenu amefunga siku yoyote ile, basi asifanye uovo wala ujinga na akimtukana yeye mtu au akimpiga basi aseme mimi nimefunga]. Vile vile Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema : “Anayekusudia kufanya hija katika miezi ya hija basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika hija].

Na vile vile ulinganizi kwa Mwenyezi Mungu ni amana. Hizi na nyinginezo nyingi ni sehemu ambazo amana hupatikana. Nikiongezea baadhi ya mambo ambayo ni katika utekelezaji wa amana ni kuwa na nguvu katika kuhifadhi haki za watu, pia katika kuwafanyia wema wazazi wawili. Vilevile ni katika amana kwa Muislamu kuchunga masikizi yake, macho na vile vile moyo wake asifanye maasi. Pia ni katika utekelezaji wa amana Muislamu kuhifadhi vyema elimu aliyoisoma. Wanavyuoni wanasema: “Hakika hii elimu ni dini basi angalieni mnaichukua kutoka kwa nani”.

Na walipokuja watu kutoka Yemen walipomtaka Mtume awape mtu wa kuwafundisha dini. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alimshika Abu ‘Ubaidah mkono na akamwambia : [Huyu ni mwaminifu wa umma huu]. Pia kuwahudumia wanaohitajia ni utekelezaji wa amana. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Nyote ni wachunga na nyote mtaulizwa kwa munachokichunga].

Pia ni katika amana kuyatekeleza aliyoamuru Mungu na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Kama ambavyo ni utekelezaji wa amana kuwaheshimu watu na kuwaweka daraja zao. Ni miongoni mwa utekelezaji wa amana ni kutoa ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hata kama ni dhidi ya mtu wako wa karibu. Pia kuwabainishia haki. Aliulizwa mwanachuoni mkubwa kuhusu babake akasema: “Baba yangu ni dhaifu”. Haya ni katika yanayohusiana na upokeaji wa hadithi. Tukijua kwamba mtu dhaifu, hadithi zake hazikubaliwi. Pia aliweza kutoa ushahidi Shu’ba ibn Hajjaj kuhusu mtoto wake: ‘Nimemwita mwanangu mzuri lakini hakuwa mzuri kitabia na hakufaulu”. Vile vile ni utekelezaji wa amana mtu kuwacha madai ya uongo kudai kuwa ana kitu fulani au anajua kitu fulani na ukweli ni kwamba hana kitu kile. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [ Mwenye kudai asicho kuwa nacho ni kama aliyevaa nguo ya uzushi]..

Mwisho

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Nawausia tunasihiane kati yetu, kwani si lengine hii Dini ni watu kupeana nasaha na mawaidha, kuamrishana mema na kukatazana maovu. Hakuna ubora wala kheri yoyote katika umma ambao watu wake hawapeani nasaha katika Dini. Na tekelezeni amana alizowapa Mwenyezi Mungu kwa wenyewe. Najueni ya kwamba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Atawauliza mlivyo vichunga siku ambayo haitomfaa mtu mali yake wala watoto isipokuwa atakayekwenda kwa Mwenyezi Mungu na moyo ulio salimika na madhambi.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Atujaalie ni miongoni mwa wenye kutoa nasaha na wenye kuzikubali nasaha na wenye kutekeleza amana alizotupa!

Vitambulisho: