tahadhari na fitna za wanawake


4659
wasifu
katika mambo alio tuhadharisha nao bwana mtume muhammad s.a.w ni fitna za wanawake,na kueleza kuwa fitna za wana waisrail ilitokamana na wanawake,na leo ndugu zangu yale alio tuhadharisha nao bwana mtume s.a.w yako wazi kabisa,wanawake wengi wamekuwa mbali na mamrisho ya allah na kuwa ni wenye kuathirika na wamagharibi,na huku hakumanishi kuwa ni wanawake wote lakini ni wengi wao kwa hivyo ni kujichunga na fitna kama hiyo
Khutba ya

Leo Mwanamke amekuwa ni bidhaa isiyo na thamani. Kila mtu anaweza kununua bidhaa hiyo kwa thamani ndogo kabisa kwa lengo la kujistarehesha, Mwanamke ni fitna kubwa katika jamii, pindi akijiweka mbali na mafundisho ya Allah. Jamii nyingi zina haribikiwa kwasababu ya maadili na tabia mbaya za wanawake. Athari ya Mwanamke ni kubwa sana katika jamii na kwa Umma wote. Katika Khutba ya leo tutaangazia suala hili muhimu la Fitna za wanawake, na jukumu la Waislamu katika kupambana na fitna hizo.

Mwenyezi Mungu ametuusia sisi na watu waliotangulia kumcha yeye. Na ushahidi wa hayo. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) katika Quraan tukufu:

قال تعالى) : وَلِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَلَقَدْ وَصَّيْنَا الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِنْ قَبْلِكُمْ وَإِيَّاكُمْ أَنِ اتَّقُوا اللَّهَ وَإِنْ تَكْفُرُوا فَإِنَّ لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَكَانَ اللَّهُ غَنِيًّا حَمِيدًا) [النساء: 131]

{{Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na kwa hakika tuliwausia waliopewa kitabu kabla yenu, na nyinyi pia kwamba mumche Mwenyezi Mungu na mkikufuru hakika ya Mwenyezi Mungu ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini na Mwenyezi Mungu ni mkwasi na mwenye kusifiwa}}.

Amrisho hilo la kumcha Mwenyezi Mungu ni kwa wote wanaume na wanawake. Lakini kwa vile wanaume ndio wasimamizi wa wanawake inapaswa juu yao kuwalazimisha wake zao juu la suala la kumcha Mwenyezi Mungu kwa njia yoyote ile iliopaswa kisheria. Ushahidi wa haya; Anasema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى: (الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَى بَعْضٍ وَبِمَا أَنْفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ) [النساء: 34] {{Wanaume ni wasimamizi wa wanawake kwa vile walivyofadhilishwa na Mwenyezi Mungu baadhi juu ya baadhi na kwa mali wanayotoa}}. Na yote hayo isipokuwa kwa sababu za kimsingi kama utoaji na utazamaji wao wa mambo kibusara. Amesema Shanqiti: Mwenyezi Mungu ameashiria kuwa mwanamume ni bora kuliko mwanamke kutokana na utukufu na ukamilifu alionao, na mwanamke ana upungufu wa kimaumbile kutokana na kujipamba.

Inafahamika kuwa wanawake waliokuwa katika zama hizi wanatofautiana na wanawake wa zama za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Mbali na wanawake wetu hawatafautiani na wanawake wasiokuwa na dini na kukhalifu miongozo ya dini kwa mfano:

Kutangamana wanaume na wanawake katika serikali kazini.

Kutangamana na wanaume katika vyuo vikuu

Kutangamana na wanaume katika masoko.

Kutangamana na wanaume katika gari za abiria.

Vyote hivyo vimeharamishwa na ushahidi wa hayo ni pindi alipotoka Musa na kuelekea Madyana kufika kisimani alikuta pote la watu wanaywesha wanyama wao na akawakuta wanawake wawili wanazuia wanyama wao wasitangamane na wanyama wengine. Akauliza sababu ya kufanya jambo hilo. Wakasema hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao kunywesha (yote hayo ni kutokana na unyonge wetu na kutopenda kutangamana na watu).

Amesema Mwenyezi Mungu kusimulia tukio hilo ndani ya Quraan tukufu: “Na alipoyafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao) na akakuta karibu yao wanawake wawili na wanyama wao akawauliza mna nini? Wakasema hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao kuchunga, na baba yetu sisi ni mzee sana”. Zingatieni msimamo huo ulinganishwe na yanayo fanyika leo.

Na katika hadithi ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Waamrisheni watoto wenu kusali hali wakiwa na umri wa miaka saba, na wapigeni wakifika miaka kumi na watenganisheni katika malazi]. Hadithi hii inamaanisha kutengamana kati ya mwanamume na mwanamke.

Na miongoni mwa ukiukaji wa maaadili ya kiislamu ni wanawake kudhihirisha mapambo yao jambo ambalo linapelekea katika uasharati kwani Mwenyezi Mungu kaamrisha kuvaa hijabu, kuhifadhi macho na kukataza kujishaua na kudhihirisha mapambo yake.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : قُلْ لِلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ذَلِكَ أَزْكَى لَهُمْ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ30 بِمَا وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آَبَائِهِنَّ أَوْ آَبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَى عَوْرَاتِ النِّسَاءِ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِنْ زِينَتِهِنَّ وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَا الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ) [النور30: 31]

{{Na waambie waumini wanaume wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao kwa unao dhihirika, na waangushe shungi zao kwa mpaka vifuani mwao, na wasionyeshe mapambo yao ila kwa wanaume zao, au baba zao, au baba za waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenziwao, au wale iliyowamiliki mikono yao ya kiume au wafuasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyokhusu ukwe wala wasipige miguu yao ili yajulikane wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi waumini ili mupate kufanikiwa}}.

 

Wamesema wanazuoni: macho ndio mlango mkubwa wa moyo, na ndiyo kuimarika kwa hisia kwa ajili hiyo tunapaswa kutahadhari nayo (macho) na kuhifadhi tupu, ima ni kujilinda na uzinifu au kuhifadhi uchi, na wasionyeshe uzuri wao isipokua kwa wale walio ruhusiwa kama Aya iliyotangulia. Imethibitu katika Musnad ya Imam Ahmad kwamba Abu Huraira amepokea hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema: (Aina mbili za watu wa motoni na mmoja wao ni mwanamke avaae nguo nyepesi isiositiri na inaonyesha uchi).

Khutba ya pili

Wanawake wema waliotangulia walikua wakijiheshimu na wakivaa hijabu na kumcha Mwenyezi Mungu, tazama kisa cha Uzushi, pindi Mama yetu ‘Aisha hakumsemesha swahaba Swafwan hata neno na hivyo ndivyo walivyo fika Madina. Na pindi walipoamrishwa kuvaa hijabu waliitikia kwa haraka wito huo bila ya kuchelewa. Ummu Salama amesimulia akisema pindi ilipoteremka Neno lake Mwenyezi Mungu: «Wateremsha nguo zao». Wamefika wanawake wa kianswaari kama juu ya vichwa vyao kuna kurabu, na wakivaa vazi jeusi Mwenyezi Mungu mkubwa kwa kuitika wito wake na wito wa Mtume wake.

Imepokewa na Ummu Salama kuwa akisema mwanamke akimwambia Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kuwa mimi ni mwanamke kurefusha vazi langu na natembea katika maeneo yenye uchafu? Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [itatwahirika baada yake]. Amesema kuwa mwanamke huyo anakusudia kuficha nguo zake pindi anapotembea kama ilivyo ada ya waarabu. Wanawake wetu na mabanati wetu wakiachwa bila ya muongozo wa dini watafanya maovu na Mwenyezi Mungu kajaalia kuwa wanaume ndio wasimamizi wao kutokana na upungufu wa akili na dini na hilo Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) anausia wanaume akisema: [Nakuusieni kuwafanyia wema wake zenu kuweni ni wasaidizi wenu].

Mwisho

Ndugu Waislamu, tumeona khatari kubwa ya Fitna za Wanawake na athari mbaya katika jamii. Ni jukumu la kila Muislamu kujitolea kubadilisha hali mbaya tunaoishi kwa sasa katika jamii yetu. Ikiwa ni mkeo, mamako, binti yako, binti wa Muislamu mwenzako, wote ni jukumu la kila Muislamu kuwafundisha wanawake maadili na tabia njema. Tukifanya hivyo, kwa hakika jamii yetu itabadilika na tutapata rehma za Allah (Subhaanahu wa Taala) pamoja na hifadhi yake kutokana na kila fitna. Namuomba Mwenyezi Mungu atulinde na fitna za wanawake, na awalinde wao na moto uumizao, Ewe Mwenyezi Mungu tupe mema hapa duniani na kesho akhera.

Vitambulisho: