tahadhari na ulimi


6045
wasifu
ulimi ni kiungo muhimu kwa mwanadamu,na kwa ulimi mtu huwa muislamu nao nikule kutemka shahada,na kwa ulimi mtu anaweza kutoka katika uislamu nao ni pale atakapo temka neno la ukafiri,kwa hivyo ndugu zangu tumetahadharishwa sana na kuchunga ndimi zetu,kuepukana na kusema urongo na kusengenya na tumeamrishwa tuwe ni watu wakusema ukweli,kwani makosa mengi ya binadamu hutokamana na ulimi
Khutba ya

Ulimi ni kiungo muhimu katika mwili wa mwanadamu. Ulimi ni neema kubwa miongoni mwa neema alizo neemeshwa mwanadamu na Allah (Subhaanahu wa Taala). Kiungo hiki ni silaha yenye makali mawili, silaha ya kusababisha mwanadamu kufaulu hapa duniani na kesho Akhera, au ni silaha ya kumuangamiza mwanadamu hapa duniani na kesho akhera.

Kumcha Mwenyezi Mungu ni njia ya kuokoka duniani na kesho akhera Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالي) : (وَمَنْ يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَلْ لَهُ مَخْرَجًا2 وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ وَمَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا) [الطلاق2: 3] {{Na anayemuogopa Mwenyezi Mungu humtengenezea njia ya kuokoka (na kila balaa). Na humpa riziki kwa namna asiyotizamia, na anayemtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtoshea. Kwa yakini Mwenyezi Mungu amekwisha kiweka kila kitu kipimo chake}}. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ni mjuzi wa kila kitu na hapitiwi na kitu chochote kilichoko mbinguni na ardhini. Tahadhari juu yetu kufanya jambo lisilomridhisha.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ushahidi juu ya yaliyopita:

وقوله) : وَسِعَ رَبِّي كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ ) [الأنعام: 80]

{{Mola wangu anakijua vyema kila kitu. Basi je, hamsikii mawaidha (hamzinduki)}}.

Ulimi ni neema aliompa Mwenyezi Mungu mja wake.

Amesema Mwenyezi

قال تعالي) : أَلَمْ نَجْعَلْ لَهُ عَيْنَيْنِ 8وَلِسَانًا وَشَفَتَيْنِ 9وَهَدَيْنَاهُ النَّجْدَيْنِ ) [البلد: 10]

{{Je hatukumpa macho mawili ? na Ulimi na Midomo miwili. Na tukambainishia zote njia mbili (iliyo njema na iliyo mbya)}}. Maiti wangapi wamesababisha vifo vyao kwa ajili ya ndimi zao. Je hawatatupwa watu motoni isipokuwa kwa mavuno ya ndimi zao. Inapasa kwa muumini kuhifadhi ulimi wake kwa hali yoyote ile na kujiepusha na kila ambalo linapingana na sheria, mfano wa kusengenya. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالي: (وَلَا يَغْتَبْ بَعْضُكُمْ بَعْضًا أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَنْ يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ) [الحجرات: 12] ( {{Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine. Je Mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliyekufa? La, Hampendi}}. Imepokewa na Barzah al-Aslamy Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Enyi mlioamini, kwa ndimi zenu, wala imani haijaingia katika vifua vyenu msiwasengenye Waislamu, wala msichunguze aibu zao na mwenye kuchunguza aibu ya muislamu Mwenyezi Mungu atafunua aibu yake na kumfedhehesha mbele ya watu].

Kuhadharishwa juu ya Fitna:

Hadithi imepokewa na Ibn ‘Abass kuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alipita katika makaburi mawili akasema: [ Maiti hawa wawili wanaadhibiwa wala hawaadhibiwi kwa jambo kubwa, mmoja wao alikuwa hajisafishi anapokojoa na mwengine alikuwa akieneza fitna].

Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Kutilia umuhimu kuhifadhi Ulimi

Kuhifadhi ulimi ndiko kumiliki kheri zote. Amepokea hadithi Mu’adh Ibn Jabal kuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Amesema: Je nisikujuze kwa mambo yote hayo zuia ulimi wako (chunga ulimi wako). Akasema. Mu’adh: Je tutahisabiwa kwa tunachokizungumza. Mtume akashangaa na kumuambia: Je hawatupwi watu motoni ila kwa mavuno ya ndimi zao”. Na alikuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akiwahimiza wake zake kujihifadhi na maneno yasiomridhisha Mwenyezi Mungu. Imepokewa na ‘Aisha nimemuambia Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) tosheka na bibi Safia kwa jambo kadha na kadha akimaanisha ya kuwa ni mfupi Mtume akamuambia: [Umetamka neno ambalo kwamba likichanganywa na maji ya baharini litachanganyika].

Hali ya Waislamu Leo kupuuza kuhifadhi Ndimi Zao

Inapatikana katika hali zifuatazo:

Maneno yasiokuwa na faida

Kuingilia jambo lisilo kuhusu.

Kuingilia heshima za Waislamu.

Ulimi mchafu

Kuomboleza katika msiba.

Ushahidi wa mambo yaliyopita amehutubu na akarefusha maneno yake mbele ya ‘Umar akasema ‘Umar kurefusha maneno ni ya shetani. Na imepokewa hadith’ kutoka kwa Abu Hureira, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Amesema: [Muislamu bora ni yule asiyeingilia mambo ya watu, na kuingilia heshima za Waislamu ni katika sifa za wanafiki]. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Ni haramu kwa ndugu yako Muislamu damu yake, heshima yake na mali yake, Muislamu ndugu yake ni Muislamu hamdhulumu wala hamkhini na akashiria katika kifua chake taqwa ni kwenye moyo]. Maneno machafu yaliyoenea katika jamii ya kiislamu leo huenda kuwa sababu kubwa ni vyombo vya habari. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Hapana kitu kizito katika mizani siku ya kiyama kama tabia nzuri na Mwenyezi Mungu anachukia maneno mabaya].

Ama kuomboleza katika msiba ni jambo la kijahilia ambalo limekatazwa, na tumeamrishwa tusubiri pindi tu tunapopatikana na msiba. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alipita kwenye kaburi na akamuona mwanamke analia akamuambia muogope Mwenyezi Mungu na usubiri, mwanamke akajibu hujali kilichonisibu wala hakujua kwamba anayejibizana nae kuwa ni Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akamwambia hakika ya subira ni katika tukio la Mwanzo.

Tahadhari Kueneza Uongo kwa Watu

Imepokewa hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema: [ Tahadharini na muongo, kwani uongo unapeleka kwa uovu, na uovu unapeleka mtu kuingia motoni, na mtu anasema uongo mpaka anaandikwa mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa ni muongo]. Na Akasema tena Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [ Uongo haufai hata kwa dhihaka]. Wala kuahidi mtu mtoto wake wala asimtimizie. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) kuamrisha waumini kuwa imara katika kupokea habari:

قال الله تعالي) : يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا إِنْ جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَأٍ فَتَبَيَّنُوا أَنْ تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَى مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ) [الحجرات: 6]

.

{{Enyi mlioamini, kama fasiki akikujieni na habari yoyote msimkubalie tu, bali pelelezeni kwanza, msije mkawadhuru watu kwa ujahili na mkawa wenye kujuta juu ya yale mliyoyatenda}}.

Khutba ya pili

Mwenyezi Mungu pamoja na Malaika wake wanaandika wanachozungumza mwanadamu. Na wao wanahifadhi amali zote za kheri na shari. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالي: (وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ10 كِرَامًا كَاتِبِينَ11 يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ) [الإنفطار: 12]

{{Na hakika juu yenu kuna wenye kuwatunza. Watukufu wenye kuandika. Wanayajua yote mnayoyatenda}}.

Na Neno lake Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

وقوله: (إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ 17مَا يَلْفِظُ مِنْ قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ ) [ق17: 18]

{{Wanapopokea wapokeaji wawili, anayekaa kuliani na anayekaa kushotoni. Hutoi kauli yoyote isipokuwa karibu naye yuko mngojeaji tayari (kuandika)}}.

Amepokea Abu Huraira kuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Kuwa Malaika wanapokezana usiku na mchana wakikutana katika swala ya alfajiri na al-asri, kisha wanakwenda wale walio kuwa ni wa usiku. Na mola akiwauliza naye akijua; mumewaacha vipi waja wangu? Wakijibu; tumewaacha wakiswali na tukawajia hali ya kuwa wanaswali].

Wito wa Kuwajibika kwa Maneno Mazuri

Kuwajibika kwa maneno mazuri ni sababu ya kufaulu na kusamehewa madhambi na kupata radhi zake Mola kwa ajili hiyo anasema Mola:

قال الله :(يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا70يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ) [الأحزاب: 71]

{{Enyi mlioamini, Muogopeni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya haki. atakutengenezeni vizuri vitendo vyenu na atakusemeheni madhambi yenu; Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila shaka amefanikiwa mafanikio makubwa}}.

Mwisho

Ndugu Waislamu, Ulimi ni kiungo muhimu katika mwili wa mawnadamu. Na kikiwa kizuri basi mwili wote huwa mzuri. Ni jukumu la kila Mislamu kuulinda ulimi wake kwa kutumia katika kuzungumza mambo ya kheri, kuamrisha mema na kukataza mabaya. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumefaidika na neema ya ulimi, na kupata radhi za Allah (Subhaanahu wa Taala). Namuomba Mwenyezi Mungu asituhisabu kwa yale tuliyoyazungumza ikiwa ni ya makosa, na kutupa ujira kwa maneno mazuri tuliyoyazungumza.

Vitambulisho: