islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


KUMI LA MWISHO KATIKA MWEZI WA RAMADHANI TUKUFU


16036
wasifu
Mwenyezi Mngu Aliyetukuka Ametuwekea ibada tukufu katika kumi la mwisho la Ramadhani, zenye kuzidisha Imani na kufanya ibada zikamilike na neema kutimia. Ibada hizi ni Zaka za Fitri na Swala ya Idi. Ametuwekea Zaka za Fitri ili zimsafishe mwenye kufungana na maneneo machafu na matendo visivyo faa na ni chakula kwa masikini, na Ametuwekea Swala ya Idi ili kudhihirisha nguvu za Waislamu na umoja wao na vile wanavyo jikusanya pamoja.
Khutba ya

Enyi Waislamu, Siku za mwezi mtukufu wa Ramadhani zinaendelea kuisha. Na hivi karibuni tutaanza kumi la mwisho. Je ndugu yangu Muislamu umejiuliza suala moja; Je nimefaidika kiasi gani na siku zilizopita? Kuwa mkweli na nafsi yako na ujifanyie hisabu ya vitendo vyako kabla hujafika siku ya kufanyiwa hisabu. Ndugu Muislamu, bado wakati upo, na fursa ya kufanya mambo ya kheri bado inaendelea.

Je umejiandaa kiasi gani na umejipangia mikakati gani katika kumi la mwisho? Kwa hakika ni siku muhimu katika umri wa mwanadamu, ndani yake kuna usiku mtukufu. Mwenye kuafikiwa usiku huo basi amepata kheri ya dunia na akhera. Na mwenye kukosa usiku huo basi amekosa kheri ya dunia na akhera. Ni khasara ilioje mtu kuishi duniani miaka mingi kisha aondoke duniani patupu bila ya kupata kheri ya dunia wala kheri ya akhera. Ndugu Muislamu tafakari na uzingatie, hujui kama utafika mwakani ili uweze kufunga Mwezi wa Ramadhani.

Watu wema walikuwa wakimuomba Allah mwaka mzima awaafikie kuweza kuzifikia siku hizi za kheri. Na wakifikiwa na siku hizi huwa na furaha nyingi, kwa kupata bahati ya kuishi mpaka kuweza kufunga Mwezi wa Ramadhani. Ndugu Muislamu Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Ametufundisha mambo mengi na ibada nyingi ambazo Muislamu anaweza kuzifanya kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allah (Subhaanahu wa Taala). Katika Ibada hizo ni kama ifuatavyo:-

Sunna za Kumi la Mwisho:

Kufanya bidii kusali swala ya usiku, na kuwahimiza watu wako nyumbani kuamka kusali pamoja na wewe. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mwenye kusimama usiku katika mwezi wa Ramadhani kwa Ikhlasi na kutarajia malipo kwa Allah. Atasamehewa madhambi yake yaliyo tangulia]. Imepokewa katika Sunna ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) likifikia kumi la mwisho alikuwa akigura matandiko yake na akijitahidi kusimama usiku na kuamsha wake zake na familia yake.

Kuzidisha juhudi kutafuta Usiku wa cheo. Usiku huu ni bora kuliko miezi elfu moja, bali ni bora kushinda vitu vyote vilivyomo duniani. Mwenye kuafikiwa kupata usiku huu basi kwahakika amefaulu na kupata kheri ya dunia na akhera. Katiak mafundisho ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kuhusu usiku mtukufu; Ni sunna kuzidisha kusoma Qur’an kwa wingi, kumsifu Allah na kumtukuza na kumsalia Mtume, kutoa sadaka. Na ni sunna kuomba dua kwa wingi. Bibi Aisha Alimuuliza Mtume: Je niombe dua gani katika usiku huu? Akamuambia sema: [Ewe Mola hakika yako wewe ni mwenye kusamehe waja wako na unapenda kusamehe. Nakuomba unisamehe].

Kufanya ibada ya I’tikaaf, nayo ni kutia nia kukaa Msikitini kwa lengo la kujitenga na watu na kukusudia kufanya ibada katika siku hizi. Alikuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) linapofika kumi la mwisho, akijitenga na familia yake na kuingia Msikitini kwa ajili ya kumuabudu Allah (Subhaanahu wa Taala). Na masahaba waliendelea kutekeleza Sunna hii bada ya Mtume kuondoka duniani.

Kusoma Qur’an kwa wingi na ikiwezekana kuhitimisha Msahafu katika siku hizi tukufu. Imepokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), ilikuwa ni kawaida yake katika siku za mwezi wa Ramadhani kukutana na Malaika Jibril kwa ajili ya kusoma Qur’an, na Jibril anamsikiliza.

Ndugu Muislamu, Siku kumi katika kumi la mwisho ni chaguo lake Allah (Subhaanahu wa Taala) kwa Umma huu. Na kwa rehma zake Ametujalia sisi kuweza kuzifikia siku hizi tukufu. Kwa hivyo, ni jukumu letu kufanya bidii kumuiga Mtume katika ibada zake zote, na kushindana katika kutafuta Usiku wa cheo (Laylatul Qadri). Tunamuomba Allah Atuajalie miongoni mwa waliochaguliwa kupata Lailatul Qadri (Usiku wa cheo).

Khutba ya pili

Ndugu Waislamu, Allah (Subhaanahu wa Taala) Anatupenda sana, na kwa mapenzi yake juu yetu ni kutujalia malipo na thawabu nyingi kwa kutekeleza ibada ndogo. Mfano Usiku wa cheo ni usiku moja, lakini thawabu zake ni nyingi kushinda thawabu za ibada katika miezi elfu moja. Angalia ndugu Muislamu, utukufu na rehma ya Allah juu yetu, lakini wengi katika Waislamu hawana khabari na neema kama hizi. Wakati unapita, siku zinapita na sisi tumeghafilika, mpaka tutakapofikwa na mauti ndio tutazinduka na hali ya kuwa muda umekwisha.

Ndugu Katika Imani, Khasara kubwa zaidi watapata wale waliofanya bidii kufunga mwezi huu na kufanya ibada mwanzo wa Mwezi wa Ramadhani, lakini wanapofikiwa na kumi la mwisho wanarudi nyuma, na kuacha kutekelza ibada na sunna za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Ni khasara ilioje kwa mtu aliyefanya bidii kuchuma mazuri, kisha akashindwa kuendelea na msimamo huo, na kushindwa kukamilisha kumi la mwisho.

Hukumu ya Ibada ya I’tikaafu:

Ibada ya I’tikafu ni Suuna. Muislamu anaweza kutekeleza ibada hiyo wakati wowote akitaka. Lakini ni Sunna iliotiliwa mkazo katika Kumi la mwisho la Mwezi wa Ramadhani. Amesema Mama ‘Aisha: Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) hakuacha katika maisha yake kufanya I’tikaaf katika kumi la mwisho la Mwezi wa Ramadhani.

Mambo yanayo lazimu kufanywa katika I’tikaaf:-

Kutia Nia kukaa Msikitini kwa ajili ya kufanya Ibada kwa lengo la kujikurubisha kwa Allah.

Kuchagua sehemu ya kukaa katika Msikiti, na kujilazimisha kubaki hapo ila kwa dharura ya kisheria, unaruhusiwa kutoka.

Kujiepusha na tendo la ndoa au njia za kupelekea kufanya tendo hilo.

Kufanya bidii kuzidisha kusoma Qur’an kwa wingi, na kuomba dua kwa wingi. Kufanya hivyo, itakusaidia kupata usiku wa cheo na kusamehewa madhambi yako.

Kujitahidi kufuata mafundisho ya Mtume katika kutekeleza lbada hii.

Mwisho

Ndugu katika imani, Umri wetu ni mfupi sana, na mwanadamu hajui kama ataweza kupata nafasi tena kufikia mwezi wa Ramadhani mwakani. Jambo la msingi ni kufanya bidii na juhudi kubwa kutafuta Usiku wa cheo ili tupate kheri ya usiku huu. Yule atakaye bahatika kupata usiku huu, kwa hakika huyo amefaulu hapa duniani na kesho akhera.

Tunamuomba Allah kwa majina yake matukufu na sifa zake njema atujaalie miongoni mwa waja wake Aliowachagua kupata kheri ya Usiku wa cheo. Tunamuomba Allah Atuwafikie kwa kufanya Ibada mbalimbali ambazo anazozipenda na anazoridhia. Tunamuomba Allah Atuwezeshe kufuata mafundisho ya Mtume Muhammad katika maisha yetu na atuingize pamoja na yeye katika Jannatul Firdaws.

 





Vitambulisho: