islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


KUTAHADHARI NA UZUSHI KATIKA DINI YA UISLAMU


7673
wasifu
Je, kuna yoyote aliyeishuhudia Hija na ukubwa wake, Imani na vile inavyotoa mwangaza, makundi mengi namna yanavyomtukuza Mwenyezi Mngu na kumhimidi? Mandhari ya Hija ni ya ajabu na ya kutisha, inawafanya Waumini wafurahi na wenye kumpwekesha wawe na nguvu, na wenye kughafilika wanashangaa.Hija ina maana gani kwenu nyinyi, enyi Waislamu!
Khutba ya

Shukrani za dhati ni za Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Aliyesema:

قال تعالى: (الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا) [المائدة: 3]

{{Leo nimewakamilishieni Dini yenu na nimewatimizia neema yangu na nimewaridhia kuwa Uislamu ndio Dini yenu}}. Na rehma na amani zimfikie Mtume wetu aliyesema: [ Atakayezusha katika jambo letu hili (Dini) ambalo si katika dini atarudishiwa mwenyewe].

Enyi waumini ! Mcheni Mwenyezi Mungu Ambaye amemtumiliza Mtume Muhammad pale walipokuwa watu wako katika upotofu wa ushirikina na kufuata dini ya baba zao potofu. Akawatoa katika ushirikina na kuwaleta katika Uislamu (Dini ya haki). Kwa Kweli, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alisubiri mengi maovu aliyotendewa na waovu mpaka Dini ikakamilika.Pia aliweza kuwatahadharisha watu na kufuata hawaa zao na kuzusha katika Dini ya Mwenyezi Mungu baada ya kuondoka yeye.

Kwa kweli uzushi katika dini ulianza punde tu baada ya kuondoka Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), kwani vipote vingi vilizuka kwa sababu ya watu kuacha Sunna ya Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na kufanya mambo bila ya elimu na kufuata matamanio ya nafsi. Na mfano wa vikundi hivyo ni Muutazila, Masufi, Khawaarij, Murjia na vikundi vyengine. Kuna ushahidi mwingi wa kushikamana na sunna na kujiepusha na bidaa. Mola (Subhaanahu wa Taala) amesema:

قال تعالى (قل إِنْ كُنْتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ( [آل عمران: 31]

{{Sema: ikiwa mnampenda Mwenyezi Mungu nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu Atawapenda na Atawasamehe dhambi zenu}}.

Pia Mola amesema:

قال تعالى: (وَمَا آَتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا) [الحشر: 7] {{Atakachowapeni Mtume kichukueni na atakachowakataza jiepusheni nacho}}. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) asema: [ Atakayezusha katika Dini yetu hii jambo ambalo halimo katika Dini basi atarudishiwa mwenyewe]. Vile vile Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) asema katika hadithi yake: [Anayejiepusha na sunna yangu si katika mimi]. Na katika hadithi nyingine Mtume anasema: [Hakika Mwenyezi Mungu Anaizuia toba ya kila mzushi mpaka ache uzushi], “[Jiepusheni na kuzusha mambo (katika dini) kwani kila uzushi ni upotofu]. Inatakiwa waumini washikamane na Sunna na wajiepusha na uzushi katika Dini. Kwani ndiko kumkubali kikamilifu Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), na pia kumtii yeye. Wala haifai kwa Muislamu kwenda kinyume na Sunna ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Ametahadharisha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) hilo aliposema:

قال تعالى: (فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَنْ تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ) [النور: 63]

{{Na wajitadhari wanaokhalifu amri ya Mtume wasije wakapata fitna au adhabu kali}}. Vilevile, Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Anasema:

قال تعالى : (وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَنْ يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَنْ يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُبِينًا) [الأحزاب: 36].

{{Haitakiwi Muislamu, mwanamume wala mwanamke atakapo amua jambo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wawe na khiari kulifanya na atakaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi amepotea upotevu wa wazi kabisa}}. Aya hizi zanaonesha kwamba yoyote atakayemuasi Mola na Mtume atakuwa katika upotevu na kupata adhabu kali ya Mwenyezi Mungu

Ndugu Muislamu kwenda kinyume na Sunna ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), ni sababu ya kufarakana Waislamu katika Dini na kupotoka upotevu ulio wazi, Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَأَنَّ هَذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَنْ سَبِيلِهِ {{Hakika njia yangu hii ifuateni wala msifuate vijinjia mtapotea( [الأنعام: 153] ( katika njia ya Uislamu}}. Vilevile, kukhalifu Sunna ni sababu ya mtu kufuata matamanio ya nafsi. Mola (Subhaanahu wa Taala) ametutahadharisha kufuata matamanio kwa kusema:

قال تعالى) : أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَهَهُ) [الجاثية: 23]

{{Je wamjua anaye yafanya matamanio yake kuwa ni mola wake}}. Na wanaofuata matamanio ni wale ambao Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Aliwataja kwa kusema:

قال تعالى : (أُولَئِكَ الَّذِينَ طَبَعَ اللَّهُ عَلَى قُلُوبِهِمْ وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُمْ ) [محمد: 16]

{{Hao ni wale ambao Mwenyezi Mungu amepiga muhuri katika nyoyo zao na wakafuata matamanio yao}}.

Uzushi katika Dini, Mtume ameuita kuwa ni upotofu kwa sababu mzushi amepotea kwa kufuata matamanio. Tusisahau Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alikuwa akijilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na tabia mbaya, na kufuata matamanio ya moyo. Enyi waja wa Mwenyezi Mungu ! Haifai kwa mtu yeyote kuleta maoni yaliyo kinyume na Sunna ya Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Amesema ‘Abdillahi Ibn ‘Abbas: “ Atakayeleta maoni ambayo hayapo katika kitabu cha Mwenyezi Mungu wala hadithi za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kwani hajui yatakayompata yeye atakapo kutana na Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Jueni kuwa mzushi ni dhalili na pia ana hasira za Mwenyezi Mungu aliyetukuka. Amesema Imam Shatwiby, Mwenyezi Mungu amrehemu: “Hakika mzushi atavishwa udhalili duniani na hasira za Mwenyezi Mungu”. Na hii ni kwa neno la Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Aliposema:

قال تعالى) : إِنَّ الَّذِينَ اتَّخَذُوا الْعِجْلَ سَيَنَالُهُمْ غَضَبٌ مِنْ رَبِّهِمْ وَذِلَّةٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُفْتَرِينَ ) [الأعراف: 152].

{{Hakika waliofanya kijing’ombe kwa muabudiwa watapata hasira za Mola wao na udhalili duniani na vile vile tunawalipa wazushi}}.

Adhabu hii itakuwa pia kwa wale wanaofanana nao kitabia kwani uzushi ni kumsingizia Mwenyezi Mungu. Asema Imam Malik Mwenyezi Mungu amrehemu: “ Atakayezusha katika Uislamu uzushi, akauona uzushi huo ni mzuri basi amedai ya kwamba Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amefanya khiana katika ujumbe, kwani Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema: “ Leo nimewakamilishia Dini yenu”. Kwa hivyo, lile ambalo halikuwa siku hiyo Dini basi leo haliwi dini’.

Na ameweka bayana Mtume kama ilivyo katika sahihi Muslim kwamba wazushi watasogea katika birika la Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na watafukuzwa kwa sababu ya uzushi wao unamaliza Dini sahihi ya Mwenyezi Mungu.

Khutba ya pili

Sababu za Uzushi katika Dini.

Ndugu zangu katika imani ! Napenda kutaja miongoni mwa sababu za uzushi katika dini.

1. Kufuata matamanio ya nafsi zao na kuacha Sunna Sahihi za Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Amesema mwanachuoni Muqaatil Ibn Hayan: ‘Watu wa matamanio ni maangamivu kwa umati Muhammad hali ya kuwa wanamtaja Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na jamaa zake wakitaka kuwavutia kwa utajo huu mzuri, watu wasiojua chochote katika Dini na kuwatia katika maangamivu, na hao wamefanana zaidi na wanaotia sumu katika asali’.

2. Kufuata baba zetu bila ya uongofu. Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema pale Nabii Ibrahim alipowaambia watu wake:

قال تعالى (قَالُوا نَعْبُدُ أَصْنَامًا فَنَظَلُّ لَهَا عَاكِفِينَ 71قَالَ هَلْ يَسْمَعُونَكُمْ إِذْ تَدْعُونَ72 أَوْ يَنْفَعُونَكُمْ أَوْ يَضُرُّونَ73 قَالُوا بَلْ وَجَدْنَا آَبَاءَنَا كَذَلِكَ يَفْعَلُونَ ) [الشعراء71: 74] {{Je mnaabudu nini? Wakasema tunaabudu masanamu na hatuachi kulazimiana nayo, akasema: Je wanawasikia mnapowaomba au wanawanufaisha au wanawadhuru, wakasema: Tumewapata baba zetu wakifanya hivyo}}.

3. Kufuata maneno ya wanavyuoni yanayokwenda kinyume na mafunzo mazuri na sahihi ya Uislamu.

Madhara ya Uzushi

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu uzushi una madhara mengi ambayo yatakiwa tuyajue. Na katika madhara hayo ni:-

Uzushi huangamiza dini sahihi huku ukichukua nafasi ya Sunna. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Hawatazua watu uzushi isipokuwa ataondoa Mwenyezi Mungu kwao Sunna mfano wake].

Ufisadi wa uzushi ni kujiepusha mtu na Sunna na akawa mtu hataki kuzifanya sunna akawa na bidii kutekeleza uzushi, na kumbe anapoteza nguvu zake na pia wakati wa huku akiaona kuwa Dini ni pungufu akitaka kuikamilisha dini na uzushi wake.

Uzushi unarejesha watu katika jahiliya kwa kuwafanya watengane wawe mbali mbali, kila kikundi kinafurahia msimamo wake. Mola (Subhaanahu wa Taala) amesema:

قال الله تعالى) كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ ) [الروم: 32]

{{Kila kikundi kinafurahia msimamo wake}}. Kwani Sunna inafanya watu kuwa kitu kimoja. Mola Asema:

قال تعالى) : وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا( [آل عمران: 103] {{Shikamaneni na Dini ya Mwenyezi Mungu wala msifarakane}}.

Uzushi unasababisha kuikataa haki anapolinganiwa mzushi katika Sunna hakubali na natija yake huendelea kushikamana na uzushi wake.

Uzushi unaharibu Dini sahihi ya Mwenyezi Mungu, kwani uzushi ndio silaha kubwa ya kuharibu Dini ya Mwenyezi Mungu. Kwani wengi katika wazushi hutaka maslahi ya kidunia katika ulinganizi wao.

Mwisho

Ndugu Waislamu ! Maswahaba walikuwa wakiwatahadharisha watu na uzushi katika Dini. Ilimfikia Ibn Mas’uud kuwa ‘Amru ibn ‘Utba ambaye ni katika wafuasi wake amejenga Msikiti mjini Kuufa akaamrisha Ibn Mas’uud uvunjwe Msikiti ule, kisha akasikia sasa wanajikusanya nje ya Msikiti huo wakileta nyiradi na adhkaar na takbira maalum kinyume na mafunzo mazuri ya bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Alifunga safari Ibn Mas’uud akawajia wao hali ya kuwa amejifunika uso wake ili wasimjue, kisha akakaa nao wakaanza kuleta adhkaar zao, kisha akafungua uso wake, kisha akawauliza mumekuwa wajuzi wa dini zaidi kuliko maswahaba wa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), Kisha akawaonya watu hao na uzushi, na hapo hapo watu waliomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu kwa uzushi wao waliokuwa wakiufanya. Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume ! Muogopeni Allah (Subhaanahu wa Taala), na mujue ya kwamba yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) yanamtosha Muislamu katika maisha yake wala asijishughulishe na chochote cha uzushi. Na wausia mshikamane na Sunna kisawasawa.

Mwisho kabisa tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie ni miongoni mwa mwenye kushikamana na Sunna na kijiepusha na uzushi na atuongoze katika Dini Yake ya sawa.





Vitambulisho: